BENKI ya Ecobank imeahidi kuendelea kulikopesha zaidi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), katika mradi wa kujenga nyumba na kukopesha ili kuhakikisha Watanzania wengi wanapata nyumba bora na za bei nafuu.
Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, James Cantamantu-Koomson, ametoa ahadi hiyo wakati baada ya hafla iliyoandaliwa na NHC kwa ajili ya kutiliana saini mkataba wa mkopo na taasisi tisa za fedha juzi jijini Dar es Salaam. Katika hafla hiyo, Ecobank ilisaini kutoa mkopo wa Sh bilioni 2.1 na imeahidi kuwa itaongeza kiasi kingine cha fedha siku zijazo ili kufanikisha mradi huo wenye manufaa kwa wananchi.
Mkurugenzi huyo alisema Ecobank inawajali Watanzania na imeahidi kuunga mkono kwa dhati mpango huo wa NHC ili kuwakomboa Watanzania wengi ambao hawana makazi bora kutokana na kipato kidogo.
“Sisi Ecobank mradi kama huu si mgeni kwetu, tunajali na kuthamini sana masuala ya makazi, karibu nchi zote 30 tunazofanya kazi zetu tunashiriki miradi kama hii, kuwapa wananchi nyumba bora ni jambo la muhimu sana,” alisema.
Ndugu Cantamantu-Koomson alisema ingawa benki hiyo ina miaka miwili tu tangu ianze kutoa huduma zake nchini, imejitahidi kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya Watanzania na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Mwishoni mwa mwaka 2011, NHC ilipewa kibali na Serikali kukopa kwenye taasisi za fedha za ndani na nje ya nchi ili kuendeleza miradi ya ujenzi
Kwa ujumla Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limesaini mikataba ya mkopo wa Sh bilioni 165 kutoka kwa taasisi nyinginezo tisa za fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miradi ya ujenzi wa nyumba pamoja na ununuzi wa ardhi ya akiba.
Taasisi za fedha zilizotoa mkopo huo pamoja na kiwango walichotoa kwenye mabano ni pamoja na CRDB (Sh bilioni 35), ECO Bank (Sh bilioni 2.1), TIB (Sh bilioni 22), BancABC (Sh bilioni 4.2), NMB (Sh bilioni 26), CBA (Sh bilioni 24), LAPF (Sh bilioni 15), Azania (Sh bilioni saba) na Shelter Afrique (Sh bilioni 23).
SOURCE http://monfinance.com/ FOR MORE INFORMATION
No comments:
Post a Comment