Hali ya Shule ya msingi SAKU iliyoko Manispaa ya Temeke
Jijini Dar es salaam si ya kuridhisha baada ya kukabiliwa na uhaba wa
miundombinu na kusababisha zaidi ya Wanafunzi 200 kusoma ndani ya chumba kimoja.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkondongwa NASORO
RASHID anasema shule hiyo kwa sasa haina madawati ya kutosha, madarasa hali inayosababisha wanafunzi wengi kusomea
chini ya miti na wengine kujazana katika darasa moja.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa
suala hilo hakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa madai kuwa yeye si msemaji huku
akifanya juhudi za kuwazuia waandishi wa Clouds kufuatilia tukio hilo.
Kitendo cha Mwalimu Mkuu kujaribu kuzuia Waandishi wa
kituo hiki kufuatilia matatizo ya Shule hiyo kinamshangaza Mwenyekiti wa
serikali ya mtaa huo ambae anasema kuwa haoni sababu ya Mwalimu kuchukua hatua
hiyo wakati shule hiyo ikiwa na miundombinu ambayo hairidhishi.
Baadhi ya wazazi wameiambia Clouds fm kwamba matatizo
yanayoikabili shule hiyo yanachangiwa pia na uongozi mbovu wa mwalimu mkuu huyo
ambae hana ushirikiano na wazazi.
Swali la kujiuliza ni kwamba kama shule iliyoko jiji la
Dar es salam inakuwa na wanafunzi wanaosomea chini kwenye sakafu na wengine
kusoma chini ya miti, Je kwa shule za vijijini zitakuwa katika hali gani, ni
vyema serikali ikalitazama hili kwa jicho la tatu.