Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu imelikataa ombi la Mawakili wanaomtetea mtuhumiwa wa mauaji ya muigizaji wa filamu nchini Marehemu STEVEN KANUMBA, ELIZABETH MICHAEL maarufu kwa jina la LULU la kutaka kesi hiyo isikilizwe katika mahakama ya watoto kutokana na mtuhumiwa huyo kuwa na umri wa chini ya miaka 18.
Akizungumza mahakamani hapo Hakimu mfawidhi AUGUSTINE MMBANDO wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, amesema ELIZABETH anakabiliwa na kosa la mauaji na mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji isipokuwa mahakama Kuu na kuwataka kupeleka ombi hilo katika mahakama hiyo.
Awali wakili wa Serikali katika kesi hiyo ELIZABETH KAGANDA baada ya kupokea cheti cha kuzaliwa cha ELIZABETH amesema ipo haja yak kufanyika kwa uchunguzi kuhusiana na umri wa mshitakiwa huyo kutokana na maelezo aliyoandika polisi wakati alipokamatwa kuwa ana umri wa miaka 18 wakati cheti hicho kinaonyesha ana umri wa miaka 17.
Wakili huyo pia amesema katika cheti hicho limeandikwa jina la DIANA ELIZABETH wakati mtuhumiwa alitaja jina lake kuwa ni ELIZABETH MICHAEL jambo ambalo mawakili wa upande wa utetezi, wamesema mara nyingi wakristo huwa wanatumia majina mawili na kudai kuwa cheti hicho ni halali.
Kesi hiyo itatajwa tena Mei 21, mwaka huu ambapo uchunguzi bado haujakamilika.
No comments:
Post a Comment