Tunapatikana Sinza kwa Remmy

Tunapatikana Sinza kwa Remmy

Monday, October 29, 2012

RAIS JAKAYA KIKWETE - ZIARA YA KILIMANJARO‏


THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425


PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
JK: Moto wa dini hautakuwa na mshindi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumapili, Oktoba 28, 2012, ameanza ziara ya siku nne kukagua shughuli na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwaambia Watanzania kuwa moto wa dini ambao umeanza kujitokeza katika Tanzania hautakuwa na mshindi.
Rais Kikwete ameanzia ziara yake kwenye Wilaya ya Same ambako amehutubia mkutano wa hadhara kwenye eneo la Stendi ya Mabasi ya mjini Same ambapo amewaambia mamia ya wananchi kuwa baada ya watu wasioitakia Tanzania mema kushindwa kuwafarakanisha Watanzania kwa kutumia ukabila sasa wamegeukia dini.
“Kuna watu hawana raha na utulivu na amani ya nchi yetu. Walijaribu kutufarakanisha kwa kutumia ukabila lakini hili lilishindikana na sasa wamegeukia dini. Lakini ndugu zangu moto wa dini hautakuwa na wa kuuzima na hautakuwa na mshindi,” Rais Kikwete amewaambia wananchi kwenye mkutano huo.


Amewataka Watanzania kuendelea na utulivu wao wa kidini na wakatae kufarakanishwa kwa tofauti za dini. “Ndugu zangu, siku zote tumekuwa na dini zetu, kila mmoja akiwa na uhuru wake wa kuabudu anachokitaka na kukiamini na kwa namna anavyotaka yeye. Ni muhimu tuendelee kuheshimu tofauti zetu za dini bila kuzigeuza tofauti hizo kuwa chimbuko na sababu ya ugomvi.”
Rais Kikwete pia amewahakikishia wananchi wa Same kuwa Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la maji katika maeneo ya wilaya hiyo na wilaya za jirani za Mwanga na Korogwe katika Mkoa wa Tanga.
Amesema kuwa mradi mkubwa wa kusambaza maji katika vijiji 34 katika wilaya hizo kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu utaanza kutekelezwa Februari mwakani. Mradi huo wenye thamani za dola za Marekani bilioni 34 utawahudumia wananchi katika vijiji 14 vya Wilaya ya Same na utachukua kiasi cha miezi 18 kukamilika.
“Tutalifanya suala hili la ukosefu wa maji kuwa historia katika Wilaya ya Same. Baada ya miezi 18 kuanzia Februari mwakani tutakuwa hatuzungumzi tena tatizo hilo,” amesisitiza Rais Kikwete huku akishangiliwa sana na wananchi hao.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa mradi mdogo wa kutoa maji ya dharura katika Wilaya ya Same utaanza kutekelezwa wiki ijayo wakati pampu za maji zitakapoletwa kwa ajili ya kufungwa.
Rais Kikwete ataendelea na ziara yake leo, Jumatatu, Oktoba 29, 2012 kwa kuzindua Kiwanda cha Tangawizi kilichoko Mamba Miamba na kufanya mkutano hadhara na wananchi.

Baadaye kesho, Rais Kikwete atazindua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Asha-Rose Migiro iliyoko Mwanga.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Oktoba, 2012

No comments:

Post a Comment