JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAARIFA KWA UMMA
MAADHIMISHO YA SIKU YA AFYA YA MACHO DUNIANI
TAREHE 11 OKTOBA 2012
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaadhimisha Siku ya Afya ya Macho Duniani ambayo huadhimishwa duniani kote kila Alhamisi ya pili ya mwezi Oktoba ya kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha jitihada za kutokomeza upofu unaozuilika duniani.
Mwaka huu siku hii itaadhimishwa tarehe 11 Oktoba 2012 katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Kauli mbiu ya Siku ya Afya ya Macho Duniani kwa mwaka 2012 ni; “AFYA BORA YA MACHO NA MAENDELEO YA TAIFA” Sambamba na kauli mbiu hii, ujumbe mahususi kwa wadau wa Afya ni; “AMUA KUWEKEZA SASA KATIKA HUDUMA ZA MACHO, UEPUSHE GHARAMA ZA ULEMAVU WA KUONA”
Kauli mbiu hii inatoa msisitizo na kuonyesha umuhimu wa wananchi kuwa na afya bora ya macho, ili waweze kushiriki vema katika shughuli za maendeleo. Aidha, ujumbe mahususi unalenga wadau wa Afya ili waelekeze juhudi zaidi na kutoa kipaumbele katika kuboresha huduma za macho nchini.
Azimio la Dira 2020 ya Kutokomeza Upofu Unaozuilika ifikapo mwaka 2020 na Siku ya Afya ya Macho Duniani
Maamuzi ya kuadhimisha Siku ya Afya ya Macho Duniani yalifikiwa na Lions Club International Foundation mnamo mwaka 1998, na baadae kuungwa mkono na wadau wengine wa Huduma za Macho ambao ni pamoja na Muungano wa mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, Serikali , wataalamu wa masuala ya afya, taasisi mbalimbali na watu binafsi.
Dira 2020 ni Azimio la Kutokomeza Upofu Unaozuilika Duniani ifikapo mwaka 2020. Azimio hili linasisitiza juu ya upatikanaji wa haki ya kuona kwa kila binadamu duniani.
Serikali ya Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani katika azimio hili mnamo tarehe 23 Mei 2003.
Malengo ya Dira 2020 ni pamoja na:-
- Kuinua uelewa wa wadau juu ya sababu za upofu unaozuilika na njia mbalimbali zinazoweza kutumika ili kusaidia kutokomeza hayo matatizo ya afya ya jamii zetu.
- Kuainisha na kuwekeza rasilimali muhimu ulimwenguni zinazohitajika ili kuziongezea uwezo wa programu za kukinga na kutibu magonjwa yaletayo upofu.
- Kuwezesha Vitengo vya Huduma za Macho kwenye nchi kupanga, kuendeleza na kutekeleza Mikakati mikuu mitatu ya Dira 2020 ambayo ni:
1.Udhibiti wa magonjwa
Mkakati huu unalenga udhibiti na tiba kwa magonjwa makuu yanayoleta upofu
2.Uendelezwaji wa rasilimali watu
Mkakati huu unalenga kuwezesha upatikanaji wa mafunzo kwa madaktari bingwa wa macho na kada nyingine muhimu zinazohusika katika kutoa huduma za macho.
3.Uimarishwaji wa Miundombinu na uendelezwaji wa teknolojia muafaka
Mkakati huu unalenga katika kusaidia kuboresha miundombinu na teknolojia ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za macho.
Dira 2020 inaweka msisitizo wa kuongeza kasi ya kutokomeza upofu unaoweza kuzuilika duniani. Utekelezaji wa Dira 2020 unazingatia na kusisitiza ugawanywaji wa jamii kwenye ‘Wilaya za Dira 2020’ yaani jamii yenye wakazi takriban milioni moja, ili kurahisisha uratibu wa shughuli za kutokomeza upofu unaoweza kuzuilika. Kila ‘Wilaya ya Dira 2020’ ambayo hapa nchini ni Mkoa ama Wilaya inatakiwa kuwa na uwezo wa kutoa huduma za macho zilizo endelevu za gharama nafuu, zinazopatikana wakati wote na za kiwango cha juu. Sambamba na huduma hizi, ‘Wilaya ya Dira 2020’ inatakiwa kutoa elimu ya afya ya macho inayolenga kuboresha afya ya macho, kuzuia na kutibu magonjwa ya macho na huduma za utengamao kwa watu wenye ulemavu wa kuona.
Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho yanalenga katika kuweka bayana na kuhamasisha wadau wote kuhusu hali halisi ya matatizo ya magonjwa na upofu duniani na huduma za Afya ya Macho ili kuwafanya waelekeze nguvu zaidi katika kukamilisha Azimio la Dira 2020.
Hali ya Ulemavu wa Kuona Duniani:
Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 285 duniani wana matatizo ya kuona. kati ya hao, milioni 39 wana upofu na milioni 246 wana uoni hafifu.Asilimia 80 ya matatizo yote haya ya kuona yanayoikabili dunia yanachangiwa na sababu zile zinazoweza kuzuilika.Idadi kubwa ya watu wenye matatizo ya kuona (asilimia 90) wanaishi katika nchi zinazoendelea.
Matatizo ya upeo mdogo wa macho kuona ambao haujarekebishwa yanaongoza kidunia kama sababu ya matatizo ya kuona wakati mtoto wa jicho anaongoza kama sababu iletayo upofu. Japokuwa matatizo ya upeo mdogo wa macho kuona ni sababu kubwa ya matatizo ya kuona kidunia, mtoto wa jicho anabaki kuwa ni sababu kuu ya matatizo ya kuona katika nchi zinazoendelea.
Asilimia 65 ya watu wenye matatizo ya kuona na 82% ya watu wasioona ni wale wenye umri wa zaidi ya miaka 50, japokuwa watu wenye umri huu ni asilimia 20 tu ya wakaazi wa dunia. Watoto milioni 19 duniani wana matatizo ya kuona.
Hali ya upofu nchini Tanzania
Kulingana na Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za hivi karibuni, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 992, 250 (yaani asilimia 3.15) wenye matatizo ya kuona ambapo kati yao, wasioona ni 315,000 (asilimia 0.7 ya wakaazi wa Tanzania). Watu wenye uoni hafifu wanakadiriwa kuwa 787,500.
Sababu kubwa zinazosababisha upofu unaoweza kuzuilika hapa nchini na dunia kwa ujumla ni:-
· Mtoto wa jicho (Cataract)
· Shinikizo la jicho (Glaucoma)
· Matatizo ya retina ikiwa ni pamoja na yale yatokanayo na ugonjwa wa Kisukari na umri mkubwa
· Upofu wa utotoni utokanao na upungufu wa Vitamini A, mtoto wa jicho, maambukizi ya surua na maambukizi ya kisonono toka kwa mama kwenda kwa mtoto
· Makovu kwenye kioo cha jicho
· Upungufu wa upeo wa Macho kuona na uoni hafifu (Refractive Errors na Low Vision)
· Trakoma/Vikope (Trachoma)
Huduma za Macho nchini
Hapa nchini Tanzania huduma za macho zinapatikana katika hospitali zote za Wilaya, Hospitali za rufaa za Mikoa, Hospitali za Rufaa za zoni, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali maalum ya CCBRT. Katika kila Wilaya na Mkoa, yupo mratibu wa huduma za macho ambaye shughuli zake zinaratibiwa na Mratibu wa Kitaifa chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Waratibu hawa ni madaktari bingwa, madaktari wasaidizi ama wauguzi waliosomea fani ya macho. Aidha katika kila hospitali ya Mkoa na Wilaya kuna wauguzi wa macho pamoja na mtaalam wa kupima upeo wa macho kuona na miwani wanaoshirikiana kiutendaji na waratibu hawa.
Huduma zinazotolewa ni pamoja na: elimu ya afya ya macho na mwili kwa ujumla, uchunguzi wa kina, upimaji wa miwani, huduma ya matibabu, huduma za upasuaji wa jicho na huduma za utengemao kwa wale wenye ulemavu wa kuona.
Huduma maalumu za macho kwa watoto zinatolewa katika hospitali za KCMC, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya CCBRT.
Aidha, huduma za macho nchini kama ilivyo huduma nyingine za afya hutolewa kwa ushirikiano mkubwa kati ya Serikali na hospitali binafsi pamoja na taasisi za kidini.
Mafanikio na changamoto
Katika miaka 12 iliyopita kumekuwa na mafanikio kadhaa yaliyolenga kutokomeza upofu unaozuilika duniani, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuyafikia malengo ya dira 2020 ikiwa imebakia miaka 8 tu kufikia mwaka huo wa 2020.
Baadhi ya Mafanikio yaliyokwishapatikana ni pamoja na:-
· Utetezi unaofanywa na wadau wa macho duniani umeweza kusababisha kuhamasika kwa viongozi na watunga sera katika nchi zote 193 zilizo wanachama wa Shirika la Afya Ulimwenguni.
· Mpango- kazi wa Udhibiti wa Upofu na Uoni Hafifu umetengenezwa chini ya uratibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni ili kusaidia taasisi zinazolenga kutoa huduma bora ya afya ya macho.
· Nchi 100 zimeshaandaa mpango-kazi wa huduma za macho.
· Jumla ya nchi 118 ulimwenguni zimefaulu kuanzisha kamati za Taifa za Dira 2020.
· Takwimu zinaonesha kwamba hadi leo, idadi ya watu wenye upofu imepungua kutoka watu milioni 45 mwaka 1999 hadi watu milioni 39 mwaka 2011.
· Idadi ya watu wenye matatatizo ya kuona yatokanayo na magonjwa ambukizi kama vile surua imepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka 20 iliyopita.
Changamoto zilinazokabili utekelezwaji wa Dira 2020 ya Kutokomeza Upofu Unaoweza Kuzuilika Duniani kote ni pamoja na:-
· Kuna upungufu mkubwa wa rasilimali watu katika utoaji wa huduma za macho
· Kuna ushindani mkubwa wa rasilimali chache zilizopo ukizingatia kuwa kuna matatizo mengineyo makubwa kama vile ukimwi, kifua kikuu na malaria. Hali hii inapelekea huduma za macho kukosa kupewa kipaumbele kinachostahili.
· Kukosekana kwa miundombinu na teknolojia kwa ajili ya utoaji wa huduma za macho kutokana na ushindani wa rasilimali.
Wito wa kiutendaji:
Ili Tanzania iweze kuchangia katika kufikiwa kwa malengo ya Dira 2020 ya Kutokomeza Upofu Unaoweza Kuzuilika ifikapo mwaka 2020, yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:-
· Halmashauri na Mikoa iweke nia na kutenga rasilimali kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa huduma za macho zinazojitosheleza katika hospitali zao.
· Mashirika ya maendeleo yaunge mkono na kuungana pamoja na Mashirika binafsi ili kuwezesha utekelezwaji wa dhana nzima ya Dira 2020.
· Wanataaluma wa fani ya Macho wafanye wajibu wao kwa kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja katika kuwezesha upatikanaji wa huduma endelevu za macho ndani ya mfumo mzima wa huduma za afya nchini.
“Pamoja tunaweza kutokomeza upofu unaozuilika”
IMETOLEWA NA
KAIMU KATIBU MKUU
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII.
No comments:
Post a Comment