Tunapatikana Sinza kwa Remmy

Tunapatikana Sinza kwa Remmy

Monday, April 9, 2012

Rais Jakaya Kikwete atoa mkono wa pole kwa Familia ya Marehemu Steven Kanumba

Rais Kikwete amefika nyumbani kwa Marehemu Kanumba eneo la Sinza, Dar es Salaam, ambako amejiunga na mamia kwa mamia ya waombolezaji, wasanii na wana-familia kuombeleza kifo cha mmoja wa wasanii vijana, hodari zaidi na wenye vipaji vikubwa zaidi katika tasnia ya sanaa.

Mara baada ya kuwasili nyumbani kwa Marehemu Kanumba, Rais Kikwete  ametia saini kitabu cha maombolezo na baadaye kuingia ndani kuzungumza kwa ufupi sana na wana-familia pamoja na wasanii wengi wa kike wa Tanzania.

Katika salamu zake za rambirambi kwa wanafamilia, Rais Kikwete amesema kwa kifupi tu: “Nimekuja kuhani msiba wa kijana wetu Steven Kanumba. Tulifahamiana sana wakati wa enzi ya uhai wake na mwaka jana nilimwalika Dodoma kwa ajili ya chakula cha mchana na wasanii wenzake wachache.

Ametutoka akiwa bado kijana sana lakini Mwenyezi Mungu ana mapenzi na uwezo wake. Nawaombeni kuweni na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba.”

Rais Kikwete pia amewaasa wasanii kuwasikiliza wana-familia katika maamuzi yote yanayohusiana na wapi azikwe marehemu. Marehemu Steven Charles Kanumba aliaga dunia usiku wa kuamkia jana, Jumamosi, Aprili 7, 2012. Alikuwa na umri wa miaka 28.



Hayati STEVEN CHARLES KANUMBA 'Mcheza Filamu'



 
Rais JAKAYA KIKWETE akiweka saini katika kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu STEVEN CHARLES KANUMBA Sinza 'Vatican' jijini Dar es salaam leo kwa ajili ya kutoa mkono wa pole kwa wafiwa.



Rais KIKWETE akiongea na wanakamati ya msiba wa marehemu STEVEN KANUMBA Sinza 'Vatican' jijini Dar es salaam alikofika kuomboleza nao kifo hicho.

No comments:

Post a Comment