Tunapatikana Sinza kwa Remmy

Tunapatikana Sinza kwa Remmy

Saturday, April 7, 2012

STEVEN CHARLES KANUMBA: NURU YA FILAMU TZ ILIYOZIMIKA GHAFLA.


Usiku wa  kuamkia   april 7 mwaka 2012 utabaki kuwa katika kumbukumbu nzito ndani ya vichwa vya Watanzania wengi wapenzi wa Filamu nchini.
Ni siku  ambayo ile Nuru kali  yenye thamani kubwa katika Tasnia ya Filamu nchini,ilipofifia  ghafla na kusababisha kiza kinene kuikumba Tasnia  hiyo ambayo imejizolea mashabiki lukuki katika kipindi kifupi nchini.

Huyu si mwingine bali ni STEVEN KANUMBA msanii  mkongwe katika tasnia ya Filamu,leo hii hatuko naye tena duniani,Baada ya kufariki duniani ghafla akiwa nyumbani kwake Sinza Vatcan Usiku wa kuamkia April 7 2012.
 Wengi tulimzoea tulimpenda,na bado  tulihitaji  kuwa naye,Lakini Mwenyezi Mungu amempenda zaidi,Na sasa hatupo naye tena.hakika amekwenda….., amekwenda moja kwa moja.


Kifo chake kimekuwa ni cha kushtusha sana, kwa sababu… KANUMBA hakulala kitandani kuugua maradhi yoyote,na wala hakupata muda wa kutoa japo hata neno la mwisho kwa watanzania,na wapenzi wa filamu zake.
Taarifa zilizopo zinaeleza kwamba umauti ulimkuta KANUMBA  muda mfupi baada ya kuanguka huku ikisemekana kuwa ni mara baada ya kusukumwa na Mpenzi wake.
Watu mbali mbali wakiwemo wasanii wa filamu walijitokeza nyumbani kwake mara baada ya kupokea taarifa za kifo chake.


Wengi tunamfahamu STEVEN KANUMBA lakini ni wapi alipotokea gwiji huyu wa filamu nchini?


Steven Charles Kanumba alizaliwa Januari 8, mwaka 1984 mkoani Shinyanga  

Elimu ya msingi alipata katika shule ya Bugoyi, na baadaye akajiunga na  sekondari ya Mwadui, kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary. 

Baada ya kumaliza Kidato cha Nne Dar Christian, Kanumba alijiunga na shule ya sekondari ya Jitegemee, iliopo jijini Dar es Salaam pia kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita ,wakati huo akiwa Jitegemee marehemu alianza shughuli za sanaa katika Kundi la Kaole Sanaa Group la Magomeni, Dar es Salaam.

Baada ya kupata mafanikio kule Kaole, Kanumba aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu ambayo nayo imeweza kufanya vizuri sana kiasi kwamba imeweza kubadilisha filamu za Tanzania hadi kutambulika nje ya Tanzania kabla ya mauti kumkuta alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima


Ameshirikiana na wasanii wakubwa duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria na amefanya kazi na mastaa wengine kadhaa wa Nigeria.
Miongoni mwa filamu ambazo alifanya ni Dar To Lagos, She is My Sister, Ancle JJ, Oprah, Tufani, Johari, Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears na kadhalika.





Marehemu stive kanumba enzi za uhai wake mbali na kuwa muigizaji mzuri katika filamu na mpenzi wa muziki pia alikuwa na ndoto za kuwa mwana siasa ambapo  alikaririwa akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Kanumba atakumbukwa na wengi sana kwa ucheshi wake- upole na ushirikiano mzuri mzuri na mkubwa baina yake na wana tasnia wenzie wafilamu lakini pia kanumba alikuwa chachu ya kuinua vipaji vya watoto wengi kutimiza ndoto zao na kuweza kuingia katika filamu tumeona mfano tu wa movie yake ya anko jj na watoto wengi wameweza kuingia katika filamu akiwemo  jenifer, Patrick na wenine wengi.

NAWEZA KUSEMA KUWA kanumba ndie msanii wa kwanza hapa nchini kupitia filamu kuitangaza Tanzania katika nchi nyingi afrika ikiwemo Nigeria ambapo mpaka  sasa wameweza kuifahamu vyema Tanzania  .

Marehemu steven kanumba  aliwahi kufika hadi Hollywood ,Marekani, ambapo alisema ameenda kutangaza vyema Tanzania katika filamu na akiwa na malengo ya kufanya filamu na wasanii wengine wakubwa huko marekani lakini kwa bahati mbaya ndoto zake hazijatimia.


Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam wakati ambapo taifa, wapenzi wa filamu, na wasanii wenzie wakisubiri tamko kutoka kwa vyombo husika kutangaza sababu ya  kifo chake.
Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu STEVEN KANUMBA.AMIN
 ============


No comments:

Post a Comment