Tunapatikana Sinza kwa Remmy

Tunapatikana Sinza kwa Remmy

Wednesday, April 18, 2012

WASHINDI WA BUNGEA LA AFRIKA MASHARIKI HAWA HAPA





Makongoro Nyerere na Adam Kimbisa, ni miongoni mwa washindi wa nafasi ya ubunge kuwakilisha katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa miaka mitano ijayo. 

Kimbisa aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na Makongoro ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, waliibuka washindi katika uchaguzi uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu ambao ulifanywa jana na wabunge wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania linaloendelea na Mkutano wa Saba mjini hapa. 

Mbali na wawili hao, washindi wengine ni pamoja na Meneja Uhusiano wa Benki ya NMB, Shy-Rose Bhanji, aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi katika Jimbo la Kawe, Dar es Salaam, Angela Kizigha na Mbunge aliyekuwa akiwania tena nafasi hiyo, Abdullah Ali Hassan Mwinyi. 


Kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi huo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, Kimbisa aliongoza kundi la Tanzania Bara, akipata kura 210 akifuatiwa na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCCA), Bernard Murunya mwenye kura 135. 
Watatu ni Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyepata kura 123. 

Miongoni wa walioshindwa katika kundi hilo ni Dk. Edmund Mndolwa, Elibariki Kingu, Evans Rweikiza, Mrisho Gambo, Mbunge wa zamani wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga, mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, William Malecela wote wa CCM na John Lifa-Chipaka (TADEA). 

Shy-Rose ambaye aliwahi kuwania nafasi hiyo miaka ya nyuma bila mafanikio, hatimaye ameibuka katika kundi la wanawake akishika nafasi ya pili nyuma ya Kizigha, kwa kupata kura 120. Kizigha alipata kura 166. 

Walioanguka katika kundi hilo ni pamoja na Fancy Nkuhi, Godbertha Kinyondo, Janet Mmari, Janet Mbene, Sebtuu Mohamed Nassor, Sofia Ali Rijaal kutoka CCM na Rose Mwalusamba (CUF). 

Kundi la Zanzibar, Abdullah ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, aliongoza kwa kupata kura 227 wakati mshindi mwingine Maryam Yahya Ussi alipata kura 91, huku vigogo kadhaa wakitupwa nje. 

Hao ni pamoja na wabunge wa zamani Dk. Haji Mwita Haji na Zuberi Ali Maulid aliyekuwa Mwenyekiti katika Bunge la Tisa. Pia wamo ni Ahmada Hamad Khatib, Khamis Jabir Makame na Dk. Said Gharib Bilal. 

Kwa upinzani, nafasi zimekwenda kwa Wakili maarufu, Twaha Taslima wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyepata kura 175 na Nderakindo Kessy wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 113. 

Miongoni mwa ambao kura hazikutosha ni Anthony Komu wa Chadema kura 93, Dk. Fortunatus Masha wa UDP kura 58, Juju Danda wa NCCR-Mageuzi kura 23, Micah Mrindoko wa TLP kura 66 na Mwaiseje Polisya wa NCCR-Mageuzi 47. Kwa mujibu wa Dk. Kashillilah, kura zilizopigwa ni 305 sawa na asilimia 87 ya wabunge wote na kura 19 sawa na asilimia 6.2 ziliharibika. Kura halali zilikuwa 286.

HABARI NDIO HIYO KUTOKA KWA VIJIMAMBO.

No comments:

Post a Comment